"Marriage is our last, best chance to grow up."

Tuesday, April 22, 2008

Honeymoon (Fungate) - 2-

Wana ndoa wapya wakiwa honeymoon {wakitembea beach}.
(Picha kwa Hisani ya Black Magazine)
Mambo ya Msingi Kuamua kuhusu Honeymoon
Honeymoon ni muda ambao wanandoa wengi huusubiria kwa hamu kubwa, ni kweli kuna raha yake kwani unatimiza moja ya ndoto kubwa duniana za kupata ubavu wako.
Kama ni kijana wa kiume naamini una subiri kwa hamu sana kwa sababu kuna nguvu katika hisia zako inakuongoza kuisubiri kwa shauku hiyo siku.
Na kama ni binti naamini unajiuliza sijui itakuwaje na kutokana na mengi unayosikia kuhusu siku ya kwanza naamini kuna wakati unahuzunika na kuna wakati unafurahi pia.

Ingawa harusi mara nyingi hushikirikisha ndugu, jamaa na marafiki katika maamuzi mengi, suala la honeymoon ni la mke na mume mtarajiwa kuamua ni wapi na kwa muda gani.
Hivyo suala la kuongelea jinsi harusi itakavyokuwa linatakiwa kwenda sambamba na jinsi honeymoon itakavyokuwa, mkizembea haitakuwepo sijui mtamlaumu nani.
Wanandoa wengi hujisahau kuzungumzia suala la honeymoon na matokeo yake hujikuta fedha zote zimeishia kwenye maandalizi ya harusi na kubakia weupe bila pesa na hivyo kusababisha kukaa honeymoon kwa siku moja au mbili tena sehemu ambayo hawaipendi.Mambo ya msingi kuamua kuhusu haneymoon yenu:
Bajeti
Ni muhimu kujua ni sehemu (hotel) gani mtaenda na bei yake itakuwaje na zaidi mnataka kukaa siku ngapi au kutumia siku ngapi kwa ajili ya honeymoon.
Kiwango cha chini kabisa ni siku mbili, ingawa wapo wamekaa honeymoon kwa siku moja naamini tatizo ni bajeti kwani wengi hujisahau.
Wengi sana hutumia siku 5 au 6 hasa kutokana na majukumu ya kazi na maisha kwa ujumla. Wapo hukaa mwezi mzima honeymoon.
Kitu cha msingi ni kukubaliana ninyi wenyewe ni muda gani mnahitaji kuwa pamoja kwa kuangalia bajeti mliyonayo.
Wapo wengi hutegemea wasimamizi wao kuwapa pesa za honeymoon, kama ni hivyo ongea nao mapema ususibiri siku ya harusi ndiyo uanze kuwauliza honeymoon itakuwa wapi.
Pia wengine husubiri fedha za zawadi ndo ziwasaidie kulipia honeymoon, uwe makini kwani unaweza kupewa zawadi za vitu bila pesa sijui utauza vitu?
Pia ni muhimu kuwa na pesa ya ziada zaidi ya bajeti kwa ajili ya dharura.

Wazo Kamili
Wengi hudhani honeymoon ni kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa kwa mara ya kwanza; na kuelekeza akili zote kwenye hicho kitendo tu.
Kumbuka, sasa ninyi mtaishi pamoja wawili kuliko muda wote mlivyoishi na wazazi wenu hivyo haina haraka kuhakikisha kwamba lazima hiyo siku ya kwanza utimizi kila kitu.
Pia huyo ni mume wako au mke wako haraka ya nini wakati ni mali yako,
Polepole ndiyo mwendo na haraka haina baraka.
Honeymoon ni mahali ambapo unaenda kupumzisha akili baada ya mikikimikiki ya maandalizi ya harusi, unaenda kukaa nakutumia muda wako maalumu na yule unampenda na kuanza uzoefu mpya wa maisha pamoja huku mkifurahia uumbaji wa Mungu.
Fikiria ni kitu gani mtakifanya zaidi ya kula na kulala.
Je, kuna mchezo wowote mtacheza kama kuogelea.
Andika vitu vile mtapenda kufanya pamoja mkiwa honeymoon vitakavyowafanya muwe kitu kimoja na zaidi sana kuwaweka karibu kujuana zaidi.
Pia Fahamu kwamba mnapoongelea suala la namna honeymoon mnataka iwe, tayari mnapata uzoefu wa maisha ya ndoa kwani kuna vitu mtakubaliana na vingine vitahitaji muda.
Chagua Sehemu
Chagua sehemu kufatana na bajeti yenu, msisubiri mpaka kila kitu cha harusi kikamilike.
Nenda sehemu mnapenda kuitumia kwa ajili ya honeymoon na fahamu bei yake fanya booking na zaidi angalia kama wanafanya punguzo kwa ajili ya honeymoon.
Kama ninyi hamna muda tumia wasimamizi wa harusi yenu au marafiki mnaowaamini ili kuhakikisha suala zima la honeymoon limekamilika kabla ya siku ya harusi yenyewe.
Visa na Passport
Kama mnaenda nje ya nchi kwa ajili ya honeymoon ni vizuri kuhakikisha passport yako haijaisha muda na pia unapata visa mapema iwezekanavyo.
Hii inatokana na kwamba baadhi ya nchi ili kupata visa unahitaji muda mwingi zaidi hasa nchi za Ulaya na Amerika hawakubari kirahisi inabidi uombe visa miezi mitatu hadi minne kabla.
Kuwa na Siri
Unahitaji kutunza siri ya wapi unaenda kwa ajili ya honeymoon.
Honeymoon ni kwa ajili yenu wawili tu si rafiki wala ndugu.
Hivyo jitahidi sana kuhakikisha kuna kuwa na siri kweli.
Hutakiwi kuwaambia rafiki zako au ndugu zako mtakuwa wapi isipokuwa wale unaoamini tu, kwani kuna marafiki hawana dogo wanaweza kuharibu honeymoon yenu kwa simu moja tu, kama unaweza zima kabisa simu za mkononi na wape muda maalumu watu muhimu kwamba wakupigie saa ngapi au muda gani.
Mawasiliano na Ratiba
Ni vizuri kuwa na ratiba kamili inayowawezesha kuwapa uzoefu wa utendaji ambao hauna utaratibu, ni muhimu kupanga jinsi mtakavyoitumia siku ya pili yake kabla ya kulala usiku, ili kila mtu ajue siku inayofuata mtaitumia vipi na pia itawapa uzoefu kama wanandoa wapya.
Unaweza kupanga muda kwamba hatafanya chochote bali kufurahi tu.
Pia ni muhimu sana kuhakikisha kila mmoja anakuwa na mawasiliano mazuri na mwenzake, kwani kabla ya hapo kila mtu aliishi mwenyewe na sasa mnakuwa kitu kimoja hivyo ni vizuri kumweleza mwenzako kila kitu unataka kufanya.
Uwepo Kwenye Honeymoon
Unatakiwa kuwepo kwenye honeymoon kimawazo, kiakili na kimwili pia.
Lazima umtangulize mwenzio kwa kila kitu hakikisha wewe unajitahidi kumfurahisha mwenzako kwa kadri unavyoweza na si kusubiri yeye akufurahishe wewe.
Sema naye, cheza naye, ongea naye na fanya vitu vingi na yeye, tumia muda wako pamoja na wewe na si kusoma vitabu, au vitu vingine.

Tutaendelea.........

No comments: