"Marriage is our last, best chance to grow up."

Saturday, April 26, 2008

Honeymoon (Fungate) - Mwisho

Ni vizuri kumkubali mwenzako kama alivyo kwa maana kwamba wewe tu peke yako hapa duniani ndiye unayeweza kuvumilia na kuchukulia udhaifu wake wote alionao, vinginevyo kila mtu akijiona bora kuliko mwenzako mnaweza kufanya honeymoon kuwa uwanja wa masumbwi.
Mambo ambayo yanaweza kuharibu honeymoon:
1. Usitegemee mwenzako afanye kama wewe unavyotaka.
Kumbuka mmekutana watu wa malezi tofauti na aina tofauti ya maisha, hivyo usitegemee sana kila unachotaka wewe mwenzio atafanya na kutimiza.
Hapo mnakutana ili tofauti zenu zianze kuunganishwa na kuwa kitu kimoja kinachofanana hivyo mnahitaji muda na uvumilivu ili kuijenga familia mpya iliyozaliwa.
Kutakuwa na tofauti kubwa katika kufikiria mambo na kufanya mambo hivyo mnahitaji kuvumiliana.
Mwingine akilala usiku amezoa kuzima taa na pia atapenda wakati wa kufanya mapenzi taa ziwe zinawaka na inaweza kuwa mwenzako ni kinyume chake yaani anaona aibu na anapenda taa zizimwe, msipokuwa na Hekima mnaweza kufikishana mbali na mkaumia.
2. Kutegemea mwenzako akupe furaha wewe.
Furaha ni kitu ambacho kipo ya ndani ya mtu, huwezi kukigusa kwa mikono, na huwezi kuchukua furaha kwenye bakuli na kuijaza kwenye moyo wa mtu mwingine, bali ni wewe mwenyewe kwanza kuwa mtu mwenye furaha bila kutegemea mwenzako awe chanzo cha furaha.
Kila mmoja akiwa na furaha automatically wote mtakuwa na furaha.
Otherwise mtangulize mwenzako kuliko kujitanguliza wewe kwa kila jambo.

3. Angalia maneno unayotamka.
Maneno unayotamka wakati huu ni muhimu sana unaweza kujenga au kubomoa, unaweza kufurahisha au kuhuzunisha, unaweza kubariki au kulaani unaweza kuongeza moto wa mapenzi au kuzima moto wa mapenzi.
Kuna wanandoa ambao wakati wapo honeymoon mwanamke alimwambia mwanaume "lakini wewe ni mzee sana hivi kwa nini ulichelewa kuoa?" mwanaume alikasirika sana na tangu siku hiyo ndoa imeingia zogo la aina yake.
Sentensi moja tu imemfanya mwanaume ajisikie anadharauliwa na mke wake tena siku ya kwanza honeymoon na sasa ndoa imeingia katika mgogoro na wanaishi tu bila mapenzi ya kweli.
Hivyo inabidi uwe makini na maneno au kauli unazotoa iwe utani au kawaida, fikiria kwanza kwani bado hamjazoeana tabia bado.
Pia usiwe mtu wa kulalamika na kulaumu kila kitu kwa kujilinda au kujiona wewe upo sahihi zaidi kuliko mwenzako.
Kumbuka kuna maneno huumiza kuliko kupigwa makofi na mangumi.

4. Usiweke kumbukumbu ya vitu mwenzio anakosea.
Jitahidi kusahau kila kitu ambacho mwenzako unaona anakosea.
Uliyempenda ni mpenzi wako sasa ila si mtu aliyekamilika hivyo kukosea ni sehemu ya maisha yake.
Isitokee akifanya kosa tena unakumbushia na kosa la nyuma, huko ni kumuumiza zaidi na atakumia zaidi kuliko kawaida.
Pia jitahidi kuahidi kitu ambacho unauwezo nacho (hasa wanaume) kwani kuna watu (hasa wanawake) wanakumbukumbu sana kwa kila ahadi huwa hawasahau kiasi kwamba ahadi yoyote isipotimizwa inakuwa nongwa.
Naamini kwa somo lote hili utakuwa na swali au maoni unkaribishwa tuweze kujadiliana zaidi.
Mungu akubariki sana.

No comments: