"Marriage is our last, best chance to grow up."

Wednesday, May 28, 2008

Kuna Ndoa Batili na Batilifu????

Kumekuwa na mkanganyiko katika kutambua maana na tofauti ya ndoa batili na ile batilifu.
Kimsingi hizi ni ndoa mbili zenye hadhi ya tofauti miongoni mwa wanandoa husika na mbele ya macho ya sheria. Kila moja ina sifa za kipekee zinazoifanya iwe na stahili ya kuitwa au kutambulika kama ndoa batili au batilifu. Hapa tatizo si sheria, bali ni elimu ya lugha ya Kiswahili katika matumizi, hasa kwa upande wa taaluma ya sheria.
Ndoa Batili
Hii ni ndoa ambayo kimsingi tangu asili yake ilishakosa sifa za kuwa ndoa kwa sababu ya kukosa moja au jumla ya vigezo vinavyohitajika kuifanya kuwa ndoa kamili.
Hii ni pamoja na vigezo vyote vinavyosimama kama mhimili wa ndoa kisheria. Hii hujumuisha vitu kama hiari katika kuingia mkataba wa ndoa kati ya wanandoa husika, jinsia za wahusika na hata mahari.
Hivi ni baadhi tu ya vitu au vigezo ambavyo ni kitovu cha mahusiano ya wawili kuwa katika hadhi ya kutambulika kama wanandoa halali. Sasa basi, endapo moja au jumla ya vigezo hivi vyote vitakosekana katika ndoa husika, basi moja kwa moja itakuwa ndoa batili, yaani isiyotambulika kisheria.
Msingi mkubwa wa ndoa hizi ni kwamba, haziwezi kusuluhishwa kwa namna yoyote kwani kwa kukosa sifa hizo za msingi zinakuwa zimepoteza hata uwezo wa kufikiriwa kisheria, yaani kuwekewa katazo na sheria ya nchi.
Mfano mzuri ni wa ndoa za watu wa jinsia moja ambazo kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, ni batili bila ya kujali kama katika ndoa hiyo wahusika waliridhiana na walifuata taratibu zote hitajika kisheria.
Ndoa Batilifu
Hizi ni zile ambazo zinachukuliwa kisheria kama ndoa halali mpaka hapo itakapotolewa amri ya kuivunja kutoka katika chombo chenye mamlaka ya kufanya hivyo, ambacho ni mahakama.
Lakini mahakama haiwezi kuamua tu kwamba ndoa fulani ni batilifu kuanzia sasa, bali huzingatia sababu na hoja zinazokubaliwa na sheria ambazo tunaweza kusema kuwa haziharamishi ndoa bali zinaiweka katika hatihati ya kuwa haramu.
Kwa mfano, endapo itatokea mmoja kati ya wanandoa akashambuliwa na maradhi ya zinaa, ndoa hii huwa ni batilifu, kwani hali hiyo inaweza kuwa sababu tosha ya kuvunjika kwake kwa ajili ya usalama wa mwenzi wake.
Hata kama wakati wa kufunga ndoa mmoja alikuwa na maradhi hayo na mwingine alikuwa hajui hilo, baada ya kujua anaweza kulalamika na mahakama ikaridhia na kutangaza kuvunjika kwa ndoa husika.
Kukataa kwa makusudi au kwa sababu za kimaumbile kushindwa kutimiliza ndoa pia kunaweza kuwa sababu ya kufanya ndoa husika kuwa batilifu, yaani baada tu ya kufunga ndoa wahusika hutakiwa kutimiliza ndoa kuashiria kuhalalisha maingiliano kati yao.
Sasa endapo mmoja wao atakataa kwa makusudi na bila sababu za msingi kutimiliza hilo, anayekataliwa anaweza kuiomba mahakama kuivunja ndoa husika baada ya jitihada za makusudi kushindwa kumshawishi kufanya hivyo.
Mahakama pia inaweza kuruhusu kuvunjika kwa ndoa husika kama baada ya ndoa kufungwa, mume anagundua kwamba mke wake ana ujauzito wa mwanamume mwingine. Mahakama italisikiliza hilo kama tu itathibika kuwa wakati wa kufunga ndoa husika mwanamume hakuwa na taarifa hiyo. Lakini endapo itathibitika kuwa alikuwa na taarifa kabla ya ndoa, lalamiko na maombi yake hayatasikilizwa.
Sababu nyingine ambayo mahakama inaikubali katika kuivunja ndoa batilifu ni kama itatokea mmoja wa wanandoa kuugua kifafa au wazimu. Kama maradhi haya yatakuwa ni ya kujirudia rudia na mwenzi wake hakulijua tatizo hili kabla, basi mahakama inatoa haki ya kutangaza kuvunja ndoa hiyo endapo itaombwa kufanya hivyo.
Lakini ikumbukwe na kuzingatiwa kuwa mahakama itahitaji kujiridhisha kuwa ugonjwa huo ni wakujirudia rudia na wala si kama aliwahi kuugua au huwa anaugua baada ya muda mrefu.
Aidha, haimaanishi kuwa pindi ikigundulika hivyo basi huwa ni sababu tosha au ni lazima ndoa husika ivunjwe, la hasa. Kama mume au mke wamekubaliana na hali hiyo, ndoa hiyo itakuwa na hadhi kama zilivyo ndoa nyingine.

Hii habari ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi
http://mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=5874
Simu 0786 809798 almajah2000@yahoo.com

No comments: