"Marriage is our last, best chance to grow up."

Thursday, June 12, 2008

Mume Amchinja Mkewe

Mauaji ya kinyama yametokea usiku wa kuamkia leo Jijini baada ya mwanaume mmoja kudaiwa kumuua mkewe kwa kumcharanga visu mwilini kutokana na madai yake kuwa eti, amekerwa na tabia ya kugawa penzi kwa wanaume wengine aliyokuwa nayo marehemu.
Mwanaume anayedaiwa kutenda unyama huo mishale ya saa 7:00 usiku wa kuamkia leo ametajwa kuwa ni Selemani Omari, 46, mkazi wa Mbagala Charambe, eneo la Kwa Padri. Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kandihabi, ndiye aliyeelezea tukio hilo la kusikitisha wakati akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu, leo asubuhi.
Amesema Kamanda Kandihabi kuwa Omari, anadaiwa kumuua mkewe aitwaye Bi. Halima Mohamedi ,36, kwa kumchoma visu mwilini na kumfanya apoteze maisha papo hapo.
Akasema baada ya kumuua mkewe, Omari alijaribu kujiua mwenyewe kwa kunywa sumu ambayo hadi sasa haijafahamika ni ya aina gani.
Akasema mbali ya kunywa sumu, pia Omari alikuwa ameshaacha ujumbe unaosomeka kuwa: ``Mimi Seleman nimefanywa vibaya na mke wangu Halima kwa kufanya mapenzi na watu wengine...`` Hata hivyo, Kamanda Kandihabi amesema hadi sasa, hali ya Omari ni mbaya na kwamba bado amelazwa katika Hospitali ya Temeke kwa matibabu zaidi.
Amesema mwanaume huyo ambaye yupo chini ya ulinzi mkali wa Polisi, atafikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya mauaji mara baada ya upelezi kukamilika. Aidha, amesema mwili wa marehemu Halima umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ya Temeke.

SOURCE: GAZETI LA Alasiri TAREHE 01/06/2008 http://www.ippmedia.com/ipp/alasiri/2008/06/10/116205.html
Na Mwanaidi Swedi , Temeke

No comments: