"Marriage is our last, best chance to grow up."

Wednesday, July 30, 2008

Ajeruhi wanandoa kwa kunyimwa penzi

Polisi wanamshikilia Leonard Nandi (25), mkazi wa Kijiji cha Safu wilayani Sumbawanga kwa tuhuma za kuwajeruhi wanandoa kwa risasi kwa kile kinachoaminika kuwa ni hasira baada ya kukataliwa kimapenzi na mmojawao.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Isunto Mantage, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika kijiji cha Nondo, wilayani Sumbawanga.
Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa alikwenda nyumbani kwa wanandoa hao na kuwajeruhi kwa kutumia risasi za bastola iliyotengenezwa kienyeji.

Alisema kuwa kabla ya tukio mtuhumiwa anadaiwa alimtaka kimapenzi Editha Namlenga (20), ambaye ni mke wa Essau Emmanuel, lakini alikataliwa. Kwa mujibu wa Polisi, baada ya mtuhumiwa kujibiwa hivyo aliahidi kuwa lazima atamfanyia kitu kibaya mwanamke huyo kwa kumkataa.
Walieleza kuwa siku hiyo ya Jumapili usiku Nandi alikwenda nyumbani kwa wanandoa hao na kukuta wamelala na kuanza kugonga mlango huku akimwita Editha lakini alikataa. Inadaiwa kuwa baada ya kujibiwa hivyo mtuhumiwa huyo alipiga teke mlango na kuingia chumbani kwa wanandoa hao na kuanza kuwapiga risasi.

Mantage alisema mwanamke huyo alijeruhiwa mguu wa kushoto kwenye paja huku mume wake akijeruhiwa kwenye mguu wa kushoto na kifuani. Alisema mtuhumiwa aliitupa bastola hiyo ndani na kukimbia kuelekea kusikofahamika lakini siku mbili baadaye alikamatwa katika msako wa Polisi uliofanyika kijijini hapo. Anatarajiwa kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazomkabili.


Source: Daily News; Wednesday,July 30, 2008 @20:06
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?id=10935
By Gurian Adolf, Sumbawanga


No comments: