"Marriage is our last, best chance to grow up."

Monday, July 28, 2008

Kuchoma daraja

Daraja lina umuhimu wake katika maisha ya kila siku.
Mara nyingi daraja hujengwa kuunganisha sehemu mbili zilizotenganishwa na mto.
Na wale ambao tumezaliwa sehemu ambazo kuna madaraja tunajua vizuri sana uzuri wa madaraja na tatizo kubwa ambalo hutokea pindi haya madaraja yanapopata matatizo kama vile Kubomoka, kuungua au kuzolewa na maji au mafuriko.

Katika suala la mahusiano pia kuna kitu kinaitwa kuchoma daraja.
Kuchoma daraja ni tabia ya kuachana na mtu katika uchumba au urafiki wa kimapenzi kwa mbwembwe za dharau kwamba humuhitaji tena na huna haja na yeye tena na hana lolote.
Kuchoma daraja ni kumdharau mtu kwamba hafikii viwango vya kuwa na urafiki na wewe kitu ambacho kinakufanya umdharau mwenzio.

Wapo ambao akina kaka au akina dada ambao hata akipata barua, au ujumbe au sms kutoka kwa kijana wa kiume au kwa dada kumtaka urafiki (mahusiano), basi hujibu ovyo au hutoa matusi kana kwamba hana haja naye au huyo kaka/dada hana maana.

Hii tabia si nzuri kwani dunia hii ni ndogo sana, ipo siku utakutana naye pale unahitaji msada wake kwani hakuna binadamu asiyemuhitaji mwingine na anaweza kuwa ni huyo unayemchomea daraja.
Tumeshuhudia watu waliochoma madaraja wakati wapo shule za msingi na ikapita miaka 10 au 15 wakaoana na kuishi pamoja na wale waliwachomea madaraja, kile kitendo cha kuchoma daraja bado kikawa kinakumbukwa hadi kwenye ndoa zao.

Kitu cha msingi hata mtu kama humpendi ni vizuri kumjibu vizuri tu akiwa anakutaka au kuomba uwe mchumba au urafiki, kwani heshima hainunuliwa ni kitu cha bure.
Matusi na dharau havifai katika dunia ya leo hata kama ni kabila ambalo hulipendi au ana sura ambayo wewe huipendi.
Wahenga walisema
"Usitukane Wakunga na Uzazi Ungalipo"

Kumjibu mtu vizuri hakuta kupunguzia kitu chochote katika maisha yako ila ukitukana watu na kuwadharau unajiharibia uzuri wako bure.

No comments: