"Marriage is our last, best chance to grow up."

Tuesday, July 22, 2008

Mapenzi na Matarajio

Tupo kwenye safari ya mapenzi, na kila mmoja anapopata mwenzi anakuwa na matarajio yake.

Inawezekana yakawa ya dhahiri au siri ya moyo wako lakini yote kwa yote ni kwamba wote maisha yetu ya kiuhusiano huyajengea picha katika fikra na kutamani iwe hivyo bila upungufu wa aina yoyote.
Katika fikra zetu, huwaumba wenzi wetu na kutaka wafanane vile tunavyotaka, huwaza mambo ambayo tunapenda watufanyie, ingawa shaka iliyopo nyuma ya mambo yote hayo ni kwamba hutokea kwa nadra sana mtu kuvuta hisia na kufikiria kumfurahisha mwenzake.

Hata hivyo, ni vema ukajua kuwa matarajio mengi huzaa mambo ambayo tunayaita ni matatizo.
Labda, swali la kujiuliza ni hili, ni kwanini matarajio yazae matatizo?

Jibu ni hili, katika matarajio kuna matokeo ya aina mbili, kutimia au kinyume chake, pia ifahamike kuwa kutotimia ndiyo zao la matatizo.

Ni kwanini matarajio?

Mwanasaikolojia Guy Finley ambaye huandika mada zake nyingi kupitia mtandao wa intaneti aliwahi kuandika:

“Kulaumu wengine kwa mateso tunayopata kila wakati, mtu kushindwa kuishi kwa matarajio, haina tofauti na kuunguza ndimi zetu kwa kahawa ambayo ni ya moto mno hata kuitema, lakini katika hilo, tunakilaumu kikombe kwamba ni pumbavu!”
Kimsingi, matarajio katika tamaduni zetu ni jambo la kawaida.
Lakini hutofautiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine.
Watu makini mambo yao huwa na mpangilio unaoeleweka, hivyo matarajio yao hutoa sauti kubwa.

Wenzangu na mimi ambao maisha yao ni rahisi kuyatafsiri kama “misingi wenyewe”, matarajio yao huwa hayana uelekeo wa kutimia, yaani ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa, muziki utachezeka?
Kuna sababu mbalimbali ambazo huchagiza matarajio kutotimia. umalaya, kuwaumiza wenzetu, hivyo kukatishana tamaa ni mambo ambayo mwanasaikolojia Larry James wa tovuti ya Love Celebration, aliyaandika kuwa ni sumu kubwa ambayo hufanya uhusiano uende ndivyo sivyo.

Kwa mfano, kama ninataraji wewe unipende katika njia moja, na penzi lako likawa halikidhi kwangu, hapo ni lazima nitavunjika moyo. Njia nzuri ni kujitahidi kupata mahitaji ambayo yatakamilisha upendo wako.

Katika hilo, ni busara kumruhusu mpenzi wako akupende kama ambavyo unataka. Hebu fikiria hili, unahitaji kupendwa katika njia moja, lakini penzi unalopewa linakuwa halina nguvu, hiyo ni ishara ya wazi kwamba matarajio hayatotimia.
Sumu nyingine ambayo husababisha matarajio yasitimie ni kutokuwa na mawasiliano ya hisia, mmoja anajua mwenzake anataka nini, lakini si ajabu mwingine akawa hajui wala hajishughulishi kutafuta. Unaona tatizo lililopo?

Ni lazima kuwe na mawasiliano. Mahitaji yanapaswa kujadiliwa. Unatakiwa kuwa muangalifu ili kuona ni mambo yapi yanatakiwa kuzingatiwa ili kuuimarisha uhusiano wako.
“Kutarajia mazuri,” ni mtazamo bora kuliko kitu kingine. Baadhi husema, “Kama unarajia mambo mazuri katika uhusiano wako, kila kitu kitakwenda barabara.” Kusema ule ukweli ni kwamba hii ni hadithi.

Hali itakwenda kulingana na wewe unavyoratibu mambo yako, na utavunjika moyo pale utakapogundua kwamba mambo hayaendi katika mpangilio ulioutaka.
Hupati yale ambayo siku zote ulitamani.

Mara nyingi huwa tunataka wenzi wetu wafanye mambo sahihi kwa ajili yetu, na pale wanapotenda yale ambayo hayakongi hisia zetu, hujawa na hasira au kuvunjika moyo.
Angalizo: “Bila matarajio, utakuwa na vitu vichache vya kukatisha tamaa!”

Imeandikwa na SHULUWA JOSEPH
Source: Mtandao


1 comment:

Anonymous said...

Ni kweli unapokuwa kwenye mahusiano huku una matarajio makubwa kutoka kwa mwenzako yasipotimia au kutekelezwa unaweza kukata tamaa zaidi na kuhatarisha mahusiano yako.

Gloria