"Marriage is our last, best chance to grow up."

Saturday, July 26, 2008

Namna ya Kutunza Wosia

BAADHI ya watu wamekuwa wakipata taharuki mara baada ya kuandia wosia, wapo walioshindwa kabisa kuelewa ni namna gani wanaweza kuutunza.
Kwa walio wengi, hii ni hoja ya kuumiza vichwa hasa kwa kuzingatia kwamba imetokea mara kadhaa kwa baadhi ya wanandugu kujitokeza na kudai kuwa marehemu alikwisha wateua kuwa wasimamizi au warithi wa mali fulani kupitia wosia wa maandishi ambao kwa bahati mbaya haujulikani ulipo.
Kwa baadhi ya familia mara kadhaa hutokea kwa watu wa aina hiyo kupewa mali au usimamizi wa mali kwa kuwa ni watu ambao huheshimika au huogopewa na wanafamilia wengine, hivyo hakuna ambaye huthubutu kumpinga pindi anapotoa maelezo kama hayo na hivyo kupoteza haki za watoto na wajane ambao wanastahili kurithi mali ya marehemu wao kisheria.
Watu wa aina hii pia hutumia udhaifu huu kwamba wosia alioachiwa na marehemu ni ule wa maneno ya mdomo ambao hata hivyo aliachiwa akiwa yeye na marehemu tu. Kwa sababu ama ya heshima kama nilivyoeleza au woga, na wakati mwingine hata ukosefu wa elimu ya sheria inayosimamia mambo ya mirathi.
Katika hali hiyo, familia nyingi huishia kukubaliana na watu wa aina hii na hivyo kumkabidhi majukumu yote yahusuyo mali ya marehemu kwa imani kuwa ndiye chaguo la marehemu.
Kwa upande wa sheria, pamoja na mapungufu kadhaa iliyonayo, haikuusahau mwanya huu kwamba unaweza kutumiwa na wajanja wachache kudhulumu watu dhaifu hasa wajane na watoto.
Kama tulivyoona katika makala zilizotangulia kuwa uhalali wa wosia wa maneno ya mdomo ni sharti utolewe mbele ya mashahidi wasiopungua wanne wawili kati yao wakiwa ni wa ukoo wa mwenye wosia na waliobaki wanaweza kuwa watu wengine mbali na ndugu.
Sasa, kwa sababu sheria imeweka msingi huo kwa wosia wa maneno ya mdomo, pia kwa upande wa pili ni msingi huo huo utumikao katika kutunza wosia husika.
Kwamba, utunzaji wa wosia wa maneno unaweza kufanywa na msimamizi aliyeteuliwa na mhusika, sambamba na mashahidi wa wosia huo, kwani hakuna namna nyingine ya kuweza kupata tamko la marehemu juu ya mali yake kwa kutumia wosia wa maneno ya mdomo, zaidi ya kuwasikiliza mashahidi na msimamizi aliyeteuliwa na mwenye wosia kupitia wosia huo.
Kwa mantiki hiyo, unaweza kuona udhaifu wa aina hii ya wosia na jinsi ambavyo unaweza kuleta usumbufu miongoni mwa wanandugu na wanafamilia wengine waliobakia, hasa ukijiuliza endapo mashahidi hao watashindwa kupatikana.
Tukigeukia upande wa wosia wa maandishi, tunajifunza pia ya kuwa ili ukubalike mbele ya jicho la sheria, ni sharti uandikaji wake ufanyike na kushuhudiwa na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika wasiopungua wawili ambao mmoja ni wa ukoo wa mwenye wosia, na mwingine anaweza kuwa mtu yeyote ajuaye kusoma na kuandika bila ya tatizo.
Mashahidi hawa wote hutakiwa kuweka saini zao katika karatasi iliyoandikiwa wosia husika sambamba na mwenye wosia.
Utunzaji wa wosia wa aina hii unaweza kufanywa kwa namna nyingi tofauti na wosia wa mdomo.
Kwanza msimamizi aliyeteuliwa kusimamia mirathi husika, anaweza kupewa kipaumbele katika kufanya utunzaji huu muhimu na yeye ajihakikishe kuwa anaweza kuutunza kwa uaminifu na bila ya shaka na hatimaye kuuwasilisha siku yoyote endapo utahitajika kufanyiwa kazi.
Lakini mbali na msimamizi huyo, wosia huu pia unaweza kutunzwa kwa kutumia taasisi mbalimbali zinazoshughulika na utunzaji wa nyaraka mbalimbali kama vile mahakama, benki, makanisa kwa Wakiristo na Misikiti kwa Waislam.
Taasisi hizi zote hujigawa katika vitengo mbalimbali ambavyo ni pamoja na vya utunzaji wa nyaraka mbalimbali ikiwamo wosia. Hivyo basi, kwa mwandikaji wa wosia, ni vema baada ya kuandika wosia wake akawajulisha watu wake wote na hasa warithi wake halali, kuwa amekwishaacha wosia ambao unaeleza maamuzi yake juu ya mali yake na mambo mengine yahusuyo familia, ambao ameuhifadhi katika moja ya taasisi hizo nilizozibainisha.
Hata kama ni wosia wa mdomo, ni vema pia akawajulisha warithi wake kuwa wosia wake huo ulishuhudiwa na akina nani, japo mara nyingi wosia wa maneno hutolewa na mwenye wosia wakati akiwa katika hali mbaya kiafya kiasi cha kushindwa hata kutambua taratibu zinazohitajika katika kuacha wosia kwa watu wake.
Si vibaya endapo atawaeleza kuwa katika wosia huo ameelekeza nini ili kuwarahisishia kazi ya kuuchambua na kuutafsiri baada ya yeye kufariki.
Source: Na Mohamed Majaliwa
Gazeti la Mwanachi
(http://mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=6112)

No comments: