"Marriage is our last, best chance to grow up."

Friday, October 10, 2008

Ulimi nao mmm!

Maneno yetu huweza kubomoa ndoa kama mmomonyoko wa udongo! Utafiti unaonesha kuwa mtu mmoja kawaida huwa na maneno 5,000 ambayo hutumia kila siku kuongea kuhusu mawazo, hisia, matukio na mahitaji mbalimbali ya mawasiliano ya kila siku.

Na hayo maneno ambayo binadamu huongea kila siku yana nguvu ya ajabu mno hata kuweza kuponya au kuumiza, kutia moyo au kukatisha tamaa, kusifia au kulaumu, kuleta uhai au kuleta kifo, kuimairsha au kudhoofisha, kuleta ukweli au kuleta uwongo, kubariki au kulaani.

Pia maisha tunayoishi ni matokeo ya kile unaongea, hivyo basi kufanikiwa kwako au kushindwa kwako katika maisha au mahusiano mara nyingi ni matokeo ya matumizi ya kinywa chako.

Pia tafiti nyingi zinabainisha kwamba kinachoelezea mafanikio na kushindwa kwa mahusinao (ndoa) si uzuri wa mapenzi au kufanana kwa wahusika au kufanana kwa vitu wanavyovipenda au uchumi au umaskini au kiwango cha elimu cha wahusika bali ni maneno wanayoongea kila mmoja kwa mwenzake.

Wapo wanandoa ambao huongea maneno ambayo ni death sentence kwa ndoa zao au ni maneno yenye mtazamo hasi (negative) kwa kila jambo katika ndoa au mahusiano yao au kila kinachoongelewa wao huchuja na kuweka katika msimamo wa negatives.
Kumbuka maneno ya aina hii yasipobadilika huwa mfano wa seli za kansa kiasi kwamba huendelea kumomonyoa ndoa au mahusiano kama mmomonyoko wa udongo na huishia kuiua kabisa ndoa.

Kama ni mwanaume unahitaji kuongea maneno mazuri kwa mke wako kwa kadri unavyotaka awe.
Acha kuongea na kuendelea kusisitiza yale anafanya vibaya, jifunze kumsifia kwa mfano:-
“Mke wangu ni mzuri, mke wangu unapendeza, mke wangu una akili, mke wangu unanifaa, mke wangu ni mwanamke wa tofauti duaniani hakuna kama wewe, mke wangu ni mtamu, mke wangu una uwezo na hekima ya ajabu”

Na mwanamke naye ni hivyo hivyo lazima uongee maneno ya kujenga ndoa si kubomoa kama vile:-
“Eti mume wangu ni mbishi, mume wangu hunisikilizi, mume wangu hunijali, mume wangu huna akili, mume wangu huna lolote, mume wangu siku hizi hunivutii, mume wangu hanipendi nk”

Maneno unayotimia kwa mwenzi wako yanaweza kuumba hisia za furaha, upendo, ukaribu, sifa, kutia moyo, kufariji, kumpa nguvu, kumuinua pia maneno yako yanaweza kuumba hisia za maumivu na hasira na hatimaye kutoana ngeu.

"Words are, of course, the most powerful drug used by mankind."

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni sahihi kabisa, na wote nadhani tumeona ndoa nyingi zinavunjika labda kwa jambo dogo tu. Labda mwenzio alitaka tu kukupa sifa lakini mwisho inakuwa maudhi. kwa sababu mwingine ametafsiri vibaya. Kwa hiyo inabidi kuwa mwangalifu unapotoa sifa au sema kitu. Pia tukumbuke ulimi hauna mfupa.

Bwaya said...

Kazi nzuri kaka. Nitapita baadae kuacha maoni katika kazi zako. Nimeipenda blogu yako.

Lazarus Mbilinyi said...

Ni kweli Ulimi auna mfupa na ulimi ni kiungo pekee katika mwili wa binadamu chenye misuli imara kuliko vyote, why? kwa sababu kile ulimi kinaongea huweza kuleta uhai au kifo. Ni kweli tuwe makini na maneno tunaongea kwa wapenzi wetu.