"Marriage is our last, best chance to grow up."

Wednesday, January 28, 2009

Mume wangu na mama yake - lao moja

Mtoto wa kiume akiwa na miaka 10 hadi 14 akawa na mama tu bila baba, huwa mtoto wa mama hata akiwa ameoa! Wapo wanawake wambao wameolewa na mume ambaye ni mototo wa mama haambiwi kitu hadi mama yake aamue na anaweza kuongea na mama yake maamuzi ya ndoa na kuacha mke kama mtekelezaji tu.

Ukweli kuwa na mume ambaye anamsikiliza mama kwa kila maamuzi ya maisha ya ndoa yenu huwa inasumbua sana kama siyo kuleta matatizo makubwa katika ndoa.
Inakuwa ngumu zaidi kwa kuwa unahitaji kutomchukiza mumeo na mama mzaa mumeo maana bila mama mkwe huyo mume usingempata.
Pia wakati mwingine mama yake (mumeo) anapoleta vurugu kwako au kukuchukia tu bila sababu au kujaribu kukuona si lolote kwa mototo wake, mumeo anatulia tu kama vile haoni na zaidi anamtetea mama yake.

Inawezekana upo kwenye uchumba, na mchumba wako (mwanaume) sasa anageuka na kusema kwamba kwa sababu ambazo mama yake hajaridhika nazo labda kabila, au ukoo au dini au elimu au basi tu si chaguo la mama, eti hamuwezi kuoana.
Usibaki kimya eti ipo siku ataacha mwenyewe au mumeo na mama yake watabadilika, unaumia bure mototo wa watu, sema usikike!

Je, njia zipi za kutumia kuishi vizuri na mume ambaye bila mama mambo hayaendi?
Kaa chini na mumeo mwambie wazi kabisa kile kinaendelea na jaribu kuhakikisha mnapata jibu (solution) kwa pamoja.
Kwa upendo na heshima zote tena kwa lugha rahisi (kama umeokoka basi huku ukiwa umefunga kwa maombi ila unatabasamu), mweleze vizuri mumeo kwamba uliolewa na yeye siyo mama yake na mwambie anavyofanya inakuumiza na toa sababu kamili inakuumiza vipi.

Uwe tayari una majibu ya nini kifanyike na mwambie ni mikakati ipi au unataka iweje halafu mwambie na yeye atoe solutions kwa hili jambo, pia uwe unamsikiliza zaidi kuliko kuongea hasa mumeo anapongea.
Pia muamue kwa pamoja nani ataenda kuongea na mama yake (kumfunga paka kengele) kama mwanamke mwoga mume anaweza kwenda mwenyewe kuongea na mama yake.

Ukifika kwa mama (wote au mmoja ambaye ameenda) kaa chini, elezea jinsi unavyojisikia au mnavyojisikia na jinsi anavyowasumbua, mpe solutions za jinsi mlivyopendekeza na pia mpe na yeye nafasi aongee bila kumkatisha anapoongea.

Tahadhari!
Kama inawezekana pata ushauri kwa mtu anayeaminika anaweza kuwa mchungaji, msimamizi wa ndoa au mtu yeyote mwenye busara na hekima katika jamii.
Wanaume wengi ambao hushikwa sana na mama zao huwa hivyo kwa sababu mara nyingi wakiwa na umri wa miaka 10 hadi 14 hawakuwa na mwanaume wa kuwa nao isipokuwa mama peke yake hivyo mwanaume yeye hajui kama ameshikwa na mama yake.
.
Pia wanaume ambao wanameshikwa na mama zao hawawezi kuweka mipaka na mama zao, hivyo inabidi asaidiwe kujua kuna mipaka mwanaume anapooa na zaidi anatakiwa aweke mipaka maana yeye ni mlinzi wa mke kimwili, kiroho na kihisia.
Mwanamke pia uwe wazi kwa mama mkwe (ingawa hii kwa jamii nyingi za Afrika ngumu sana) mwambie tabia ipi inakuchukiza anapokuwa na mwanae na tabia ipi unafurahia kwani huko pia ni kuweka mipaka.

Ikiwezekana kama mnaishi jirani hama kabisa angalia uwezekano wa kuhamia mbali au umbali kidogo au mji mwingine au kijiji kingine huko unaweza kupata amani na pia unaweza kupata muda wa kukata mzizi unaomshika mumeo kwa mama yake.
Umbali wakati mwingine hufanya maajabu.

Pia mwanamke uwe umejiandaa kupata resistance kutoka kwa mumeo au mama yake, na wote wakigoma usikate tamaa pia unaweza mwenyewe kwenda kupata ushauri kupambana na hii hali.
Pia fahamu kwamba kuna wanaume (piga ua) hatakubali kujirekebisha, ila kuna mtu mmoja tu anaweza kuwabadilisha wanaume duniani yeye anaitwa ni change agent, anaweza kuleta mabadiliko yoyote, miaka 200o iliyopita alikufa msalabani kwa ajili ya wanaume na wanawake wote, mwambie yeye anaweza, jina lake anaitwa Yesu

No comments: