"Marriage is our last, best chance to grow up."

Monday, March 29, 2010

Je, Niachane naye?

SWALI

Habari ya kazi kwanza nashukuru kwa kutuelimisha kupitia blog yako.

Mimi naitwa Ishita nimeolewa,

Siku chache baada ya ndoa yetu baada ya kutoka honeymoon niligundua kuwa mume wangu ana mtoto nilisoma kwenye simu yake na ndio kwanza mtoto alikuwa na wiki moja.

Kabla ya sisi kuoana tulikuwa tunaishi pamoja kwa zaidi ya mwaka mmoja. Nilipomuuliza mara ya kwanza alikataa,

Lakini baadae alikuja kukubali na akaniomba msamaha, kwa vile nampenda sana mume wangu na yule mtoto hana hatia nilimsamehe na nikamwambia mtoto akiwa mkubwa akamchukue ili tuishi nae akakubali.

Lakini cha kushangaza na kinachoniuma mimi ni kwamba kila akitaka kumpeleka mtoto kliniki yule dada aliyezaa nae anataka aende na mume wangu kliniki na huwa namruhusu mume wangu ampeleke mtoto wake cliniki lakini roho yangu huwa inaniuma sana na isitoshe nahisi bado wanaendelea na uhusiano wa kimapenzi naomba ushauri nifanyeje na hapa nilipo ni mjamzito.

Je, niombe talaka niachane nae?

Au niendelee kuvumilia maumivu?

MAJIBU:

Dada Ishita,

Pole sana kwa shida, tatizo na machungu unayopitia.

Ni kweli Inaumiza sana, kitendo cha kuingia kwenye ndoa mpya na kukutana na shughuli nzito kama hii, kweli inaumiza sana na inaaibisha mbele za wanaokuzunguka.

Upo sahihi kabisa kujisikia vile unajisikia, kwani jambo hili huumiza, hutisha, hukatakata moyo na kukufanya ujione kama hufai kwa wazazi, ndugu, marafiki na watu wote wanaowazunguka.

Ni kitendo kinachoumiza sana kwani mwanaume uliyemwamini na kuchukua risk ya kuishi pamoja mwaka mzima bila ndoa na baada ya kukuingiza kwenye ndoa unajikuta kumbe hukuwa mwenyewe bali kuna mwingine ambaye tayari amesha mpa first born; inatisha na inaumiza sana.

Dada Ishita, kumbuka mume wako kuwa kuzaa na mwanamke mwingine ni matokeo ya ubovu wa mahusiano yenu tangu siku zile mmekubaliana kuishi pamoja bila ndoa.

Kuvutana na kuishi pamoja maana yake hakuna commitment, hakuna agano, hakuna kifungo ni kuishi kwa kubahatisha na matokeo yake mtu anakuwa huru kufanya kile anataka kwa kuwa anajua hakuna commitment.

Sasa maji yamemwagika na kilichopo ni kutafuta njia na namna ya kupata maji upya.

Kumbuka vile unajisikia hutajisikia milele ingawa ni kweli trust uliyonayo kwake huiwezi kuwa kama siku ya kwanza ulipokubaliana naye kuishi pamoja na mwenye kukuthibitishia kwamba amebadilika ni yeye mwenyewe.

Kuachana ni kama kuruka majivu na kukanyaga moto, ni kutafuta matatizo mapya magumu zaidi hasa kama hujui mzizi wa hili tatizo.

Hapo kwanza una mimba na una safari ndefu na ndoa bado mpya kabisa achana na wazo la talaka kwanza hadi utatue tatizo lililopo kwa kushirikiana na mume wako.

Na inawezekana ukiachana naye unaweza kwenda kuolewa na mwanaume mwenye sifa kama hizo tena na hali ikawa mbaya zaidi kwako.

Angekuwa mume wako alikuwa na uhusiano na huyo mwanamke na hakuna mtoto, issue ingekuwa asiwasiliane na huyo mwanamke milele, ila suala la mwanaume kuwa na mtoto na mwanamke nje ya ndoa ni suala gumu sana si katika ndoa yako tu bali ndoa zote ambazo hukutana na tatizo hili chini ya uso wa dunia.

Kwanza hawezi kukwepa responsibilities za kuwa baba kwa huyo mtoto na si haki kabisa mtoto kukosa haki zake kwa baba yake halisi.

Kuna wanawake wengi sana duniani na Tanzania wamejaa sana ambao wanahangaika na watoto kwa kuwa wanaume waliowazalisha na baadae wamewatelekeza watoto wasio na hatia, huyo mtoto hakuomba kuletwa duniani imetokea tu na hana kosa, pia anastahili kuwa na baba ambaye anahusika katika maisha yake mia kwa mia.

Hii ina maana kwamba ukitaka (pia unastahili) kuendelea kuishi na mume wako inabidi ukubali kwamba hili tatizo ni lenu wote na si yeye peke yake na huyo mwanamke na huyo mtoto hivyo shirikiana naye bega kwa bega tena kwa upendo (hata kama unaumia kiasi gani) ili kupata majibu sahihi ya kwanza namna ya kumtunza au kumlea huyo mtoto na pili ili wewe mwenyewe upone maumivu.


Bila kushirikiana wewe na mume wako itakuwa ngumu sana kwa mume wako kuwa na upendo wa kweli kwa mtoto wake na pia kwako.

Pia bila mume wako kuongea na wewe kwa uwazi, kwa akili na busara ili wewe ujue chanzo cha affair yake hadi kupelekea kupata mtoto (pia achunguzwe vizuri isije akawa ana mtoto mwingine sehemu zingine tena) na pia ashirikiane na wewe kutoa misimamo na namna atakavyolea mtoto na namna atashirikiana na huyo mwanamke na wewe kuhakikisha mtoto anapata haki zake na ndoa yako na yeye inaendelea.

Pia huyo mwanamke unatakiwa umfahamu na anatakiwa kutambua kwamba ninyi ni mume na mke na atambue mipaka yake na ashirikiane na ninyi namna ya kumlea huyo mtoto kiumbe kisicho na hatia.

Pia mume wako anatakiwa asimame mbele ya mshauri wa ndoa, au wazazi au watu wenye ndoa imara ambao wanaweza kuwasaidia kuwashauri.

Kutokana na tatizo lililopo; mume wako amekusababishia kidonda kikubwa sana moyoni, hivyo jiandae kukabiliana na hasira, ukali, kukosa hamu ya tendo la ndoa, kuwa na msongo wa mawazo, na inaweza kuchukua muda mrefu zaidi ya unavyotegemea kurudi kwenye hali yako ya kawaida.

Kama una maswali zaidi naomba tuwasiliane kupitia email ifuatayo:

lazarusmbilinyi@gmail.com

4 comments:

Anonymous said...

Nashukuru kwa ushauri wako, kuhusu kumfahamu huyo mwanamke aliyezaa naye. Ninamfahamu huyo mwanamke na wakati akimpeleka klininki huyo mtoto japo kuwa roho inakuwa inaniuma sana lakini najikaza kwa sababu kama ulivyosema mtoto yule hana hatia. Huwa tunakwenda wote cliniki mimi, mume wangu na huyo dada. Kwa kweli naumia sana ila nakesha nikimwomba Mungu anipe roho ya uvumilivu.

Kwa sasa hivi upendo kwangu na mume wangu umepungua na hata tukiwa tunafanya mapenzi AM not feeling anything Am doing just as my responsibility but sifurahii lile tendo hata nikijitahidi nimeshindwa sometimes nawaza labda kwa vile nina mimba ndio maana sijisikii kufanya mapenzi au sababu ni hali iliyojitokeza. Sometimes nafikiria nimwambie yule dada kuwa aache kuendelea na uhusiano wa kimapenzi na mume wangu kwa sababu mara nyingi akimpeleka mtoto kliniki tunakuwa pamoja lakini naona kama itakuwa ugomvi na mimi kati ya vitu ninavyovichukia ni ugomvi. Je nimweleze yule dada ukweli au ninyamaze wasiwasi wangu asije akazaa nae tena mtoto mwingine. Kwa kweli hata mimi swala la kuachana na mume wangu nilimpenda na kumzoea naona kama ndio nitakuwa nimejiongezea matatizo zaidi. Samahani kwa kukusumbua ila naomba ushauri zaidi.

Mimi Ishita

Lazarus Mbilinyi said...

Dada Ishita,

Kwanza hongera sana kwa namna ulivyobarikiwa kuwa na upendo wa tofauti kwani si rahisi kwenda na mume wako huku upo na mwanamke aliyezaa naye, upo tofauti sana!

pamoja na mengi tumeongea jambo la msingi kwanza lazima ufahamu mzizi wa affair ya mume wako, ndiyo umemsamehe na mtoto aliyezaliwa hana kosa je, unajua ilitokeaje hadi akazaa naye? huwezi kuzuia asizae naye tena kama hujui kile kilipelekea azae naye mara ya kwanza.

Pia ni suala la wewe na mume wako katika ushirika kama timu, kama wanandoa kuongea na huyo mwanamke kumueleza ukweli kwamba ninyi ni mke na mume na anatakiwa kuheshimu mipaka ya ndoa yenu vinginevyo mnaweza kujikuta mpo kwenye mitala.
Itakuwa vema sana kama mume wako ndiye atakuwa anamweleza huyo mwanamke ikiwezekana mbele ya mshauri wenu wa ndoa.

Unavyojisikia kuumia upo sahihi na ni haki yako na pia kutokuwa na hisia wakati wa tendo la ndoa ni sahihi kwani hiyo inatokana na namna yeye ameuharibu moyo wako na moyo wako umezikalia akili zako kiasi kwamba hakuna moto 9passion) wa mapenzi tena na it is his fault na lazima ajitahidi ili trust irudi tena.

Ubarikiwe

Upendo daima

Anonymous said...

yaani ndoa jamani, sijui ni kitu gani, yaani wanaume hawa, mimi nina mume wangu ambaye ukiniambia kwamba anaweza akacheat ningeweza kukubishia mpaka mwisho, lakini amecheat tena mbaya zaidi amempa mimba huyo mwanamke, yaani mtu unalia mpaka unajuta ni kwanini umeolewa, maana kwa mkristo ndo hauna choice tena, hata ukienda kwa mwingine naye atacheat tu one day, yaani haya maneno ya kusema jiulize ulichofanya akacheat, itakuwa kuna jambo, haya maneno imefika mahali tuyaangalie vizuri. maana mtu unampenda, unamheshimu, unampa kila anachohitaji bado anacheat, ukimuuliza niambie walau sababu anabaki nilipitiwa, ni shetan tu lakini nakupenda mke wangu sitaki tuachane. kwa kifupi hili suala halina suluhisho, Mungu aturehemu na atusaidie tu.

Lazarus Mbilinyi said...

Dada Anony hapo juu,

Nashukuru sana kwa maoni yako ukweli ni kwamba kila ndoa ipo tofauti na kila mwanaume na mwanamke wapo tofauti.

Kwa upande wako upo sahihi kabisa kwamba kuna wanaume haijalishi unampa mapenzi kiasi gani, unampa kila anachohitaji kiasi gani, au unajitoa kwake kiasi gani, au unampenda kiasi gani, au na yeye anakupenda kiasi gani na zaidi haijalishi haonekani kama anaweza ku-cheat kiasi gani bado akitaka kuchepuka anachepuka, ni mwanaume ovyo (jerk).
Wapo wanawake pia kwenye ndoa wa aina hii kwani hawa hawana gender, wana pattern yao ambayo huwa na tabia ya kujirudia ambayo huumiza ni kama hawana emotions za ku-control mambo yao, pia hawana ability ya kuangalia mambo katika perspective ya mtu mwingine.
Ni watu wa ajabu sana kwani vitendo vyao wakifanya shetani ndiye husingiziwa.

Kuwa na partner wa aina hii ni risk kubwa na jambo la msingi ni kumuomba Mungu (creator) aweze kumbadilisha kwani sisi kama binadamu hatuwezi kufanya lolote.

Ingawa kweli kuna wengine hutoka nje kwa sababu ndani wamekosa kile wanakitafuta nje.

Upendo daima