"Marriage is our last, best chance to grow up."

Tuesday, June 1, 2010

Je, Kuna Msaada Wowote!

Kaka,

Mimi nilizaliwa katika familia ambayo ilikuwa ni balaa (abusive) kimwili, maneno (matusi) na kimapenzi. Haikuwa sehemu nzuri kuishi na kulelewa, nilipofika miaka 10 mama yangu aliachwa na akaolewa na mwanaume mwingine ndipo kaka wa kambo mwenye miaka 19 akaja kuishi na mimi.

Nilizoea kupigiwa kelele na wakati mwingine kuzabwa vibao na huyu kaka na akawa ananiingiza chumbani kwake na kunibaka na aliniambia nisimwambie mtu kwani anaweza kuniua na pia alikuwa ananiahidi kunipa fedha ambazo hata hivyo hakunipa.

Nilipofika umri wa miaka 20 niliondoka nyumbani (toroka) na kuendelea na maisha yangu mwenyewe na nilikata mawasiliano na familia yangu na sasa nimeolewa katika umri wa miaka 30.

Mume wangu ni kijana mzuri sana ananipenda na ninapenda sana kumpa upendo na mapenzi ya uhakika hata hivyo ninajiona ni vigumu sana kushiriki tendo la ndoa, siwezi kuondoa picha zinazojirudia katika akili yangu namna nilivyokuwa nabakwa na kaka yangu wa kambo wakati nipo mtoto, nikiwa kwenye tendo la ndoa huwa najisikia kichefuchefu na hata kutapika kitu kinachonifanya kuepuka tendo hili.

Sina namna na sijajua mume wangu ananichukulia vipi,

Je, kuna msaada wowote?

Ni mimi Niliyeumizwa!

Dada Uliyeumizwa,

Kwanza pole sana kwa aina ya maisha uliyopitia na hongera kwa kuamua kumchukua hatua ili kushughulikia hili tatizo.

Ni kweli umepitia katika jambo zito sana pamoja na juhudi yako ya kuanza ukurasa mpya bado umejikuta matukio ya zamani yanaendelea kukuwinda katika maisha yako.

Jambo la msingi ni kuanza kubadilisha mtazamo wako na kuanza kuangalia mahusiano yako kiafya zaidi ingawa itakuwa ni kazi ngumu na itachukua muda kwani ni jambo linalohusisha hisia zako na kwamba kile kitendo kimekuwa imprinted kwenye asili yako ya ndani kitu ambacho itahitaji ushirikiano wako na huyo mume wako anayekupenda.

Unastahili pongezi kubwa kwa ujasiri wa kuweza kuiweka issue kama hili juu ya meza na fahamu kwamba kile kilitokea hukusababisha wewe (Not your fault), hukusababisha kutokea ila ilitokea kwa sababu huko nje kuna mijitu miovu, inayoumwa kiakili na haina hata mishipa ya fahamu ya kile inafanya kwa viumbe visivyo na hatia. Ingawa abuse uliyopata ilihusu suala la sex hata hivyo haina maana kwamba unatakiwa kukwepa sex na kuona ni kitu kibaya kwani Mungu aliumba sex kwa ajili ya wewe na mume wako kufurahia na kujileta karibu yaani mwili mmoja.

Pia ni jambo la kutia moyo sana kwamba umeoana na mwanaume ambaye anakupenda na unampenda ambaye unaweza kumwambia hii siri kwa kuwa unamuamini na unajiona upo salama kwake.

Sasa ni wakati wa kurejesha uhusiano mzuri wa kimapenzi na mume wako, ongea na mume wako, mwambie namna unavyompenda na kwa nini unajisikia vigumu kushirikiana naye katika tendo la ndoa, muombe akusaidie na awe mvumilivu wakati huu unapoponya majeraha ya yale ulipitia, mwambie kila kitu bila kumficha jambo lolote.

Pia tafuta mshauri ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndoa na mapenzi (therapist) ili aweze kukusaidia kuanza upya namna ya wewe kushirikiana na mume wako katika sex kwa upya na raha zaidi.

Hii inaweza pia kusababisha kutojihusisha na sex kwa muda fulani ili kukusaidia wewe kurudi kwenye hali ya kawaida ambapo unaweza kufurahia kushikwa na mume wako na pia kuendelea na tendo la ndoa bila kujiona unaumizwa.

Jambo la msingi ni wewe na mume wako kuwa na lengo moja pamoja, ni wakati ambao ninyi wawili mnahitaji kuwa wavumilivu na wapole kila mmoja kwa mwenzake ingawa hili jambo litakuwa emotional bado mnatakiwa kujenga mtazamo mpya wa kufurahia kama Mungu alivyoweka tangu mwanzo.

Je, unaweza kusahau kabisa hiki kitendo?

Huwezi kusahau kabisa kwani hayo maumivu ya hiyo abuse yameandikwa kwenye kumbukumbu za ubongo wako jambo la msingi unaweza kuponywa na kurejesha mahusiano mazuri ya kimapenzi na mume wako.

Pia Mungu anaweza yote, hivyo ni jambo la msingi kumuomba Mungu aweze kukupa mtazamo mpya wa maisha kimapenzi na mume wako.

1 comment:

Anonymous said...

Kaka yake sijui atubu vipi Mungu wangu!!!