"Marriage is our last, best chance to grow up."

Wednesday, November 10, 2010

Nataka Anioe!

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 25 nimependana na mwanaume mwenye miaka 30. tumekuwa pamoja miaka 3 sasa ingawa kila mtu anaishi kwake. Binafsi nina mtoto wa miaka 3 ambaye nilizaa na mwanaume mwingine bila kuoana.
Huyu mwanaume wa sasa ameniambia ananipenda na ana mpango wa sisi kuoana kwa ndoa kanisani na tumeshaenda kwa ndugu zetu pande zote kutambulishana ingawa kila mmoja anaishi kwake.

Tatizo lililopo sasa nina mimba yake na sipendi kuzaa mtoto mwingine nje ya ndoa (out of wedlock) na kila nikimuuliza huyu mwanaume ana mpango gani kuhusiana na ndoa hanipi jibu wazi na kamili huku akiishia kuniambia nimuamini na nimwachie kila kitu kwani anajua ni nini kinanitatiza na kwamba hataniangusha kwa hilo.
Sipendi aniache na sipendi kuzaa nje ya ndoa tena kwani ni aibu sana kuzaa watoto wawili wote nje ya ndoa.
Naomba ushauri nifanye nini ili anioe (kwa ndoa ya kanisani) kabla sijazaa.

Dada Jane (siyo jina haisi)Dada Jane,
asante sana kwa swali lako na pole sana kwa yale unapitia hata hivyo swali lako linaonesha umeruhusu roho ya kukata tamaa na kukubali hofu na mashaka kukutawala hata umefika humuamini mpenzi wako.

Unachotakiwa kufanya ni kuacha kumlazimisha akuoe kwa ndoa ya kanisani na badala yake onesha upendo na uvumilivu na kuwa mwanamke mwenye subira.
Kutokana na maelezo yako inaonekana mwanaume uliye naye ni mwanaume ambaye anakupenda na amejitoa kwako (committed) kwani kitendo cha kukutambulisha wewe kwa wazazi wake ambao ni watu muhimu kwake ni kuonesha anakupenda na anakujali.

Kukwambia hatakuangusha hii ina maana hapendi kwenda kichwa kichwa kwenye suala la ndoa na kwamba mpe muda kwani anajua una mimba kwani ni wewe nay eye siku ile mliamua pamoja kutengeneza mtoto na si bahati mbaya bali kwa pamoja mlikubaliana na kama ulikuwa hupendi kuzaa kabla ya ndoa usingekubali kufanya mapenzi na badala yake ungesubiri.

Kitendo chako cha kumsukuma au kumlazimisha mfunge ndoa ili kuondoa aibu ya kuzaa tena nje ya ndoa inaweza kuwa tatizo zaidi na hata maafa. Ni vizuri kumpa heshima huyo mwanaume wako kwa kumpa muda ili afanye maamuzi sahihi kama kweli unahitaji mahusiano yenye afya.

Huhitaji kutawaliwa na hofu na mashaka wakati huu muhimu kwako hasa wakati huu unapotegemea kupata mtoto mwingine, unaweza kuharibu afya yako na afya ya mtoto tumboni bure.

Mwanaume uliyenaye anahitaji muda na kujipanga namna ya kuishi na wewe na huyo mtoto ambaye si wake na huyo ambaye yup tumboni mwako.

Ndoa imara hujengwa katika misingi ya upendo, uvumilivu, ukweli na kuaminiana na si kusukumana kwani kama maji yalishamwagika.

Upendo daima.

1 comment: