"Marriage is our last, best chance to grow up."

Sunday, August 21, 2011

Usijaribu!

SWALI:

Hello mimi ni dada ninayeishi Iringa nina umri wa miaka 18 kwa bahati mbaya mpenzi wangu amenipa mimba na kutokana namna alivyo baba yangu Naamini akifahamu kwamba nina mimba ataniua Kwani mimi ni mwanafunzi.

Nimeongea na boyfriend wangu tumekubaliana tukaitoe.

Hata hivyo bado najiuliza kama kutoa mimba (abortion) ni kitu sahihi?

Na je, nifanyeje Kwani nipo kwenye njia panda.

MAJIBU:

Mdogo wangu pole sana kwa yaliyokukuta hasa kitendo cha kujiingiza kwenye masuala ya mapenzi badala ya kukomaa na shule kwanza.

Sikufichi umeshachanganya mambo na kuna gharama utalipa kwa maamuzi yako uliyoyafanya.

Jambo la msingi ni kwamba sidhani kama kuna anayehusika na utoaji mimba anayeweza kukwambia ukweli kuhusiana na kutoa mimba (abortion)

Kutoa mimba ni uuaji (murder) na kutoa hiyo mimba kutakufanya uishi kama muuaji sawa na wauaji wengine wanaoua watu na hiyo hatia itakaa moyoni mwako miaka yako yote hapa duniani.

Ukweli ni kwamba kovu la hisia za kutoa mimba zitakuwinda maisha yako yote na hatia (guilt) hutisha.

Utajisikia huzuni, hasira pale ikitokea mtu anaanza kuzungumzia suala la utoaji mimba (abortion) pia unaweza kujikuta una hisia mbaya unapowaona watoto wadogo hasa wale watakaokuwa umri sawa na yule mtoto uliyemuua kwa kutoa mimba yake pia unaweza kujikuta hapendi kabisa kushika watoto au kuwagusa watoto wenye umri sawa na yule ambaye angekuwa mtoto wako.

Ulipokuwa unafanya mapenzi na huyo boyfriend wako uliamua, na hamkutumia njia yoyote ya kuzuia mimba na ulijua wewe na boyfriend wako kwamba hicho kitendo kinaweza kusababisha mimba, hivyo basi wewe na boyfriend wako mnawajibika kwa ajili ya kuhakikisha huyo mtoto (kiumbe kisicho na hatia) anatunzwa tumboni na kuzaliwa salama na mnamtunza kama wazazi.

Pia ufahamu kwamba madhara ya kutoa mimba ni zaidi ya unavyofikiria, kuna wanawake hupoteza maisha wakati wa kutoa mimba na wengine huugua kiasi cha kufa.

Inawezekana ni kweli baba yako atakasirika sana kusikia una mimba, pia Naamini mzazi mwenye busara hawezi kumuua binti yake kwa kuwa ana mimba ya mjukuu wake. Naamini baba yako atakasirika na mwisho atakusamehe.

Kama ulikuwa unawaza kwamba siku moja utakuwa na mtoto baada ya ndoa au harusi kubwa, ni muhimu na busara kuanza kufuta hayo mawazo na badala yake tunza hiyo mimba na mtoto atazaliwa na maisha yataendelea kama kawaida.

Hakuna Tatizo linalotokea hapa duniani ambalo ni jipya yote yalikuwepo na maisha yanaendelea.

Inawezekana katika kutoa mimba ukapoteza kizazi au uzazi na siku moja ukaolewa na kushindwa kupata watoto na utajisikiaje utakapomwambia mume wako mpenzi kwamba huweza kupata mimba kwa kuwa ulimuua mtoto ambaye alikuwa tumboni mwako?

Inawezekana kwako kupata hiyo mimba ni bahati mbaya, hata hivyo mbele za Mungu huyo mtoto si bahati mbaya (accident) bali ni mpango wa Mungu kwamba azaliwe duniani na mtoto kama mtoto hana kosa ila wewe na boyfriend wako.

Je, ingekuwaje kama wazazi wako nao wangekuua ungali tumboni mwa mama yako?

Jiulize ni namna gani wangekosa unavyocheka, unavyo smile, unavyotoa machozi, unavyowapenda na vitu vyote vinavyowapa furaha ya maisha.

Achana kabisa na wazo la kutoa mimba.

Kumbuka kutoa mimba ni dhambi ya uuaji na hapa Tanzania pia ni kosa

1 comment:

Lazarus Mbilinyi said...

Ile kumaliza kujibu swali hili nikaenda kulala na usiku saa saba na nusu jirani yangu akanipigia simu kwamba anaomba msaada nimpe usafiri kwenda Hospitali ya Kibena (Wilaya ya Njombe) akamchukue mke wake.
Kumuuliza kulikoni, akaniambia binti yao anayesoma kidato cha nne alikuwa katika harakati za kutoa mimba kwa mtu ambaye si daktari (mama wa shughuli za kutoa mimba hapa mjini Njombe na alimuweka vijiti 3 ndani ya uke ili mimba itoke). Binti alizidiwa kwani mimba ina miezi saba na ndipo akapelekwa kibena jioni.
Madaktari walifanikiwa kutoa hivyo vijiti 3 na ukweli ni kwamba usiku ule tayari alikuwa katika uchungu wa kuzaa na uke ulishafunguka sentimita 3 naamini kufika asubuhi mtoto atakuwa amezaliwa.
Nilienda na rafiki yangu tukamchukua mke wake na kumrudisha nyumbani na binti aliachwa hospitalini akiendelea na harakati za kujifungua mtoto ambaye atakuwa na miezi 7.
Cha kushangaza nymba nzima walikuwa hawajui kama binti ana mimba hadi hiyo jana.
Je aliwezaje kuficha mimba ya miezi 7?
Hata hivyo ameshapoteza nafasi yake ya kufanya mitihani ya kidato cha 4.
Inahuzunisha!